Nyoyo zina njia zake sita. Tatu katika hizo ni ovu,
na tatu nyengine ni njema.
Zilizo ovu, siku zote;
- Zinapambiwa na dunia, au
- Zinaidanganya nafsi yake na Kuadhibika katika dunia, au
- Huwa zina adui anayezijaza wasi wasi na kuisababishia adhabu hiyo.
Ama njia tatu njema, ni zile
- Zinazotenda mema na kuonekana natija yake, au
- Zenye kuwa na akili inazoziongoza, na
- Zenye kumjua Mola wake ili zimuabudu kama anavyopaswa kuabudiwa.
Nyoyo zote zinatembea katika njia hizi.sita.
Kufuata matamanio ya nafsi, na kuwa na matumaini ya
kuishi muda mrefu, ni
katika sababu kubwa ya kufisidika kwa moyo, na
kufuata matamanio ya
nafsi kunasababisha kuupofosha moyo huo usiweze
kuuona ukweli na usiweze kuiona haki.
Kufuata matamanio ya nafsi kunamfanya mtu asipate
raha, na siku zote hupenda
kujishambulia au kushambulia wenzake.
Kuwa na tamaa ya kuishi mda mrefu hapa duniani,
kunamfanya mtu aisahau
akhera yake na kumzuwia asijitayarishe nayo..
Mwenyezi Mungu anapomtakia mja wake kheri, humjaalia
kuwa ni mtu
anayekubali kuwa yeye ni mtenda madhambi na kujizuwia
kufuatilia madhambi ya
wenzake.
Humjaalia pia asipende kuwanyima wenzake kile alicho
nacho katika mambo ya kheri, na kutopenda kufuatilia vya wenzake.
Na iwapo Mwenyezi Mungu hamtakii mja wake kheri, basi
huyageuza mambo, na kuyafanya yawe kinyume na hivyo.
Mtu anapoiona kheri katika nafsi yake, basi amshukuru
Mwenyezi Mungu.
Ama anapoona kinyume cha hivyo, basi ailaumu nafsi
yake.
Kwa hivyo mtu anatakiwa ajaribu kuzijuwa zile sifa
njema ili aweze kuzifuata na kuzipenda.
Na pia anatakiwa atambuwe neema alizopewa na Mola
wake ili aweze kumshukuru
kwa kuongeza utiifu.
SIFA ZA NAFSI YA HALI YA JUU
Shaqiyq Ibrahim Al Balkhiy, mmoja katika wanavyuoni
wakubwa aliyefariki katika mwaka wa 194H. alisema;
"Watu
wa aina sita hufungiwa milango ya kufanikiwa;
Wanaojishughulisha na neema wakasahau kumshukuru
aliowaneemesha.
Wenye kujishughulisha kutafuta elimu kisha
wasiifanyie kazi.
Wepesi wa kufanya madhambi na wazito wa kutubia.
Wanaopenda kufuatana na watu wema wakaacha kufuata
mwenendo wao.
Wanaoikimbilia dunia na hali dunia inawakimbia, na
Wanaoikimbia akhera wakati akhera inawakimbilia
wao".
Ama Ibnil Qayim, yeye anasema;
"Yote
hayo yanatokana na kutokuwa na uoga - uoga wa kumuogopa Mwenyezi Mungu - na asili
yake hasa ni upungufu wa yakini na upungufu wa ilimu - ilimu ya kumjua mtu Mola
wake, na asili yake hasa ni mtu kuwa na nafsi dhalili na nafsi duni inayokubali
kubadilisha kile kilichokuwa duni kwa kile kilichokuwa bora, ama sivyo kama
nafsi ingekuwa tukufu inayojiheshimu, basi isingeridhika na kilichokuwa
duni".
Heshima Ya Nafsi
Anaendela kusema Ibnil Qayim;
"Kwa
hivyo asili ya kheri yote imo katika kuiheshimu mtu nafsi yake hiyo na katika
kuitukuza kwake na katika kuitakasa kwake. Na asili ya shari yote imo katika
kuidharau mtu nafsi yake na katika kuiviza na katika kutoiheshimu.
Mwenyezi Mungu anasema;
"Bila
shaka amefaulu aliyeitakasa (nafsi yake) Na bila shaka amejikhasiri aliyeiviza
(nafsi yake)".
Suratush shams - 9-10
Na maana yake aya hii ni kuwa; 'Imefuzu nafsi ya yule
aliyeilea katika kumcha Mungu na katika kuitakasa na katika kuikuza kwa kumtii
Mwenyezi Mungu. Na imekula hasara nafsi ya yule aliyeilea katika kumuasi
Mwenyezi Mungu na katika kuichafua na kuidogosha.
Kwa hivyo nafsi zinazojiheshimu haziridhiki isipokuwa
kwa yaliyo matukufu na yaliyo bora na yenye mwisho mwema. Na nafsi zilizo duni
ziku zote zinayazungukia zungukia yaliyo duni na kuyaangukia kama nzi
wanavyoangukia uchafu.
Kwa ajili hiyo nafsi zinazojiheshimu haziridhiki na
dhulma wala haziridhiki na uchafu wala wizi wala khiyana. Na hii ni kwa sababu
nafsi hizo ziko juu na zimetakasika mbali kabisa na
mambo kama hayo.
Ama nafsi dhalili zisizojiheshimu zinakwenda kinyume
kabisa na hayo, kwani kila nafsi inaelekea kule inakopendezwa nako.
Na hii ndiyo tafsiri ya kauli yake Subhanahu wa Taala
aliposema;
"Sema;
"Kila mmoja anafanya (amali yake) kwa njia yake."
Bani Israil -84
Yaani anafanya kazi kwa njia ile anayonasibiana nayo,
kwani anafanya kufuatana na vile anavyopenda na kunasibiana na mwenendo na
tabia zake. Na kila nafsi inakwenda katika njia yake na mwenendo wake
inaoupenda na kuuelekea.
Kwa hivyo mtu asi anafanya amali zile zinazonasibiana
na mwenendo wake katika kuzilipa neema alizoneemeshwa nazo kwa uasi na kwa
kwenda kinyume na yule Aliyemneemesha. Na Muislam aliyeamini kikweli anafanya
amali zake zinazonasibiana na mwenendo wake katika kumshukuru na kumpenda yule
Aliyemneemesha, na pia katika kumsifia na kumtukuza na kumuadhimisha na
kujipendekeza kwake na kumuonea haya pamoja na kuchunga asimuasi. "
na MUHAMMAD FARAJ SALEM AL SAIY
Post a Comment